
Dragusin kukosa msimu uliobakia
Beki wa Tottenham Hotspurs, Radu Dragusin anakaribia kukosa msimu uliosalia baada ya kuumia kano ya mbele ya goti lake la kulia.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 alipata jeraha hilo wakati Tottenham iliposhinda Elfsborg kwenye Ligi ya Europa wiki iliyopita na inabidi afanyiwe upasuaji.
Anatarajiwa kuwa nje kwa angalau miezi sita na baadhi ya majeraha ya ACL yanaweza kuwaweka wachezaji nje ya uwanja kwa hadi mwaka mmoja.
Tottenham ilisema Dragusin "atafanyiwa tathmini na timu yetu ya madaktari ili kubaini ni lini atarejea mazoezini".
Dragusin alianza mechi 21 kati ya 23 zilizopita za Tottenham. Akiandika kwenye Instagram, nje, Dragusin alisema atafanya bidii wakati wa kupona kwake "kurejea akiwa na nguvu zaidi".
"Kandanda haikufundishi tu jinsi ya kushinda - inakufundisha jinsi ya kupigana wakati mambo yanapokuwa magumu."
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Romania anaungana na Destiny Udogie, Guglielmo Vicario, James Maddison, Brennan Johnson, Timo Werner, Wilson Odobert, Cristian Romero na Dominic Solanke pembeni, huku mabeki wenzake Micky van de Ven na Ben Davies wakiwa wamerejea uwanjani hivi karibuni.
Siku ya Jumapili, Tottenham ilimsajili beki wa Austria Kevin Danso kwa mkopo kwa muda uliosalia wa msimu huu, na chaguo la kumnunua lenye thamani ya £21m.
Siku ya Jumatatu, walikuwa na ofa ya £70m kwa mlinzi wa Uingereza Marc Guehi iliyokataliwa na Crystal Palace, lakini wakamsajili mshambuliaji Mathys Tel mwenye umri wa miaka 19 kutoka Bayern Munich.